Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amehidi kushirikiana na chuo kikuu cha sokoine cha Kilimo SUA katika kusaidia kufanya mageuzi kwenye kilimo hususani ufugaji.
Kauli hiyo ameitoa kwenye ziara yake ya siku moja chuoni hapo tarehe 20/10/2017 iliyokuwa na lengo la kujifunza mbinu mbalimbali za ufugaji na kilimo bora ili kuongeza ufanisi kwenye shamba lake.
Mhe. Kikwete aliahidi kuzungumza na balozi pamoja na taasisi ya AGRA (Alliance for Green Revolution in Africa) ambayo yeye ni mjumbe wake ili kuona uwezekano wa kujenga maabara za kuboreshea uzalishaji wa ng’ombe ili kupata mifugo bora yenye sifa zinazohitajika.
“Kuna nchi nyingi duniani ambazo zimefanikiwa kuzalisha maziwa kiasi cha lita 50 kwa ng’ombe mmoja kwa siku. Nilipoulizia namna ya kupata mbegu hizo niliambiwa inamlazimu mtu kusafirisha ng’ombe wazima kuwaleta nchini. Lakini kama tutatumia njia zingine za kisayansi tunaweza kupata mbegu kwa kuanzisha Sex semen lab au Embrio transfer lab” Alisistiza Mhe. Kikwete.
Alisema kuwa kwenye shamba lake anafuga ng’ombe wa maziwa 400 lakini wanaotoa maziwa ni 41 pekee na hii ndiyo sababu iliyomfanya aje kuonana na wataalamu wa SUA ili kujua anakosea wapi na afanye nini ili aweze kupata maziwa mengi na kuleta tija aliyoikusudia.
Aidha, alisema akiwa nchini China alikutana na Profesa Mmoja ambaye kwa kushirikiana na wenzake wamezalisha aina fulani ya majani ya Ng’ombe mazuri sana kwa mifugo. Aina hiyo ya majani tayari imeshafika kwa wafugaji wa nchini Rwanda. Hivyo ni muhimu wafugaji wa Tanzania nao wakapata mbegu hiyo kwa sababu wapo tayari kushirikiana na serikali yetu ili kufikisha majani hayo hapa nchini.
Katika hatua nyingine Mh. Kikwete alikubali kushirikiana na SUA katika kutumia shamba lake kwaajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa SUA na kwa namna hiyo watamsaidia kuboresha zaidi shamba lake. Ameahidi kujenga sehemu nzuri kwaajili ya wanafunzi watakaoenda shambani kwake ili wapate mahali pazuri pa kukaa katika kipindi wanapokuwa kwenye mafunzo shambani hapo.
Akizungumzia kilimo cha mananasi ambacho pia amekuwa akikifanya katika eneo la Kiwangwa alisema, mananasi yanayolimwa nchini kwetu na wakulima katika maeneo mbalimbali hayavuki mipaka kuuzwa nje ya nchi yetu.
Mhe. Kikwete alisema katika ziara zake nje ya nchi aliambiwa kuwa aina ya mananasi yanayotakiwa kwenye soko la duna ni aina ya MD2. Hivyo amewataka watafiti nchini kusaidia kupatikana na aina hiyo ya mbegu ili watanzania nao waingize mazao yao kwenye soko la kimataifa.
Rais huyo mstaafu wa awamu ya nne alisema alishangaa kuona katika nchi nyingine mananasi yanapatikana kwa mwaka mzima wakati nchini Tanzania mananasi yanapatikana kwa msimu mmoja. Kuna kila sababu kwa wataalam kutafiti kuhusu mbegu hiyo kwa kutumia njia za uzalishaji miche kwa njia ya chupa (Tissue Culture) ili iweze kupatikana kwa wingi nchini.
Awali Makamu mkuu wa chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda alimpongeza Dkt. Kikwete kwa kuchukua uamuzi huo wa kutaka kujifunza na kuichagua SUA kama sehemu ambayo anaamini wataweza kumsaidia kupata elimu aliyoikusudia.
Pia alimpongeza rais huyo mstaafu kwa jitihada zake ambazo amekuwa akizifanya katika kujiendeleza kwenye sekta ya kilimo kabla na baada ya kustaafu. Hivyo, Prof. Chibunda amemwomba Mh. Kikwete kuandaa mhadhara mkubwa na wanajumuia wa SUA kuzungumza nao ili kuwavutia watu wengi zaidia kujihusiha na kilimo.
Prof. Chibunda, akizungumzia kwa ufupi shughuli za Chuo alisema kuwa SUA kimejikita kwenye maeneo mengi katika kusaidia kutoa elimu kwa wakulima kupitia njia mbalimbali. Kupitia mpango mkakati, SUA tunanataka kuongeza jitihada za kukipeleka Chuo kwa wananchi kwa kufanya tafiti kwa wakulima ili wajifunze kwa urahisi.
“Tunafanya tafiti za ufugaji wa samaki na kuboresha sekta hiyo nchi nzima kwani tunaona uhitaji mkubwa wa samaki kwenye jamii. Uvuvi haramu unazidi kupunguza samaki kwenye maeneo mengi hivyo kama chuo tunajitahidi kutafuta njia nzuri za kuongeza upatikanaji wa samaki’’ Alisema Prof. Chibunda.