Katika kuhakikisha Elimu itolewayo na SUA inawafikia wadau wengi hasa wakulima na wafugaji, Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) inaendelea kujiimarisha katika kutoa huduma bora za ugani kupitia vipindi vya SUATV na SUAFM Radio.
Akizungumza katika kikao cha kamati ya ugani ya SUA (SUA Outreach Committee), Kaimu Mkurugenzi, Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (Institute of Continuing Education- ICE) Dr. Innocent H. Babili alisema Chuo kinakamilisha utaratibu wa kurusha vipindi vya SUATV kupitia ving’amuzi vingi zaidi ili kuwafikia wadau wengi na hivyo SUA kuchangia katika kuboresha mbinu na kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo na ufugaji.
Aidha kitengo cha SUAMEDIA, ambacho ni sehemu ya ICE, kimeanza kupanua huduma zake kwa kushirikiana na wadau wengine hususani radio Clouds FM na TBC FM ambazo zimekuwa zikirusha vipindi vya SUAMEDIA kwa lengo la kukitangaza Chuo na shughuli zake nchini.
Katika kuhakikisha kuwa SUAMEDIA inakuwa na vipindi vingi vya kitaaluma na vyenye ushawishi wa mabadiliko ya teknolojia kwa wakulima na wafugaji, Kamati ya ugani ya SUA imewataka watafiti na wakuu wa ndaki, shule kuu, taasisi, vituo, idara na vitengo mbalimbali kushirikiana kwa karibu na SUAMEDIA katika kutengeneza vipindi ambavyo vitarushwa kupitia SUA TV na SUA FM.
Kupitia SUAMEDIA, watafiti na wafanyakazi wa SUA, wanapata fursa ya kukipeleka chuo kwa jamii na hivyo kuchochea maendeleo ya kilimo na ufugaji nchi nzima, Alisema Babili.