Waziri wa katiba na sheria Prof. Palamagamba Kabudi ameupongeza uongozi wa Chuo Kikukuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa jitihada zake inazozifanya za kupanua wigo na kozi zinazofundishwa chuoni hapo na mkakati wake wa kukipeleka chuo kwa jamii ili kunufaika na matunda ya tafiti na teknolojia zinazozalishwa chuoni hapo.
Pongezi hizo amezitoa wakati akizungumza na viongozi wa chuo alipotembelea chuoni hapo na kuelezwa kwa ufupi kazi zinazofanywa na chuo pamoja na mikakati ambayo chuo kimejiwekea katika kutoa elimu bora,kufanya tafiti na uvumbuzi wa teknolojia zinazowasaidia wakulima kuongeza uzalishaji mazao na kusaidia nchi kupata malighafi za kulisha viwanda.
Prof. Kabudi alisema mpango wa chuo hicho wa kufundisha masomo mengi katika nyanja mbalimbali ndio mfumo ambao unatumiwa na vyuo vingine vikubwa duniani katika kuongeza wataalamu lakini pia kusaidia watu wanaosomea taaluma mbalimbali kukutana na kubadilishana uzoefu badala ya kujifungia kila wataalamu kwenye vyuo vyao.
Hata hivyo alipongeza jitihada za chuo katika kufikisha elimu na matunda ya tafiti kwa wananchi na jamii nchini kwani kutasaidia wananchi kunufaika kwa haraka na uwepo wa vyuo hivyo badala tofauti na sasa ambapo vyuo vingi tafiti zake zinatumika kuwapatia watu shahada na kisha kubaki kwenye makabati na kushindwa kuwafkia wananchi na wahitaji hasa vijijini.
Waziri huyo wa katiba na sheria alisema SUA ni chuo mahari kuliko hata vyuo vingine Tanzania na Afrika Mashariki kutokana na kuwa na wataalamu wengi wenye ujuzi mkubwa ambao wakitumika vizuri wanaweza kukifanya chuo kupata manufaa makubwa kwenye kubuni mbinu mbalimbali za uzalishaji mali na ujasiliamali.
Aidha Prof. Kabudi alishauri viongozi wa chuo kukibadilisha kuwa cha kijasiliamali kwa kuzalisha mali na kutoa bidhaa mbalimbali kupitia wataalamu wake lakini pia kuwawezesha wanafunzi kujifunza na wakati huo huo kujipatia kipato kupitia kilimo kwenye mashamba ya Chuo na kuboresha maisha yao wakati wakiwa shuleni.
Waziri huyo wa katiba na sheria alisisitiza kuwa kilimo ndio injini ya ya uchumi na SUA ndio wasukuma injini hiyo kwa kushirikiana na vyuo na vituo vingine vya utafiti. Taasisi hizi zikifanya kazi yake vizuri vitakuwa na mchango mkubwa sana katika kuisaidia serikali ya awamu ya tano ya kujenga Tanzania ya viwanda kwa kuwezesha wakulima kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda.
Awali akitoa maelezo mafupi ya Chuo, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Prof. Raphael Chibunda alimueleza waziri kuwa hivi sasa chuo kinafanya maboresho makubwa katika idara na ndaki zinazounda Chuo hicho ili kuweza kutoa mchango wa kutosha katika kusaidia kuinua sekta ya kilimo nchini.
Alisema miongoni mwa mipango hiyo ni kuboresha mashamba ya chuo kwa kuwa na shamba la kisasa ambalo litakuwa linamazao ya aina mbalimbali ambayo yanalimwa kisasa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi lakini pia kutoa nafasi kwa jamii kutoka pande zote za nchi kuja kujifunza kilimo na teknolojia za kisasa katika mashamba yenye hadhi ya Chuo Kikuu.
Prof. Chibunda alisema wakati serikali ikihimiza uandikishwaji mkubwa wa wanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari kwa kutoa elimu bure hakunabudi maandalizi yafanyike kwenye vyuo vikuu kuweza kuhimili idadi kubwa ya wanafunzi hao ambao wanatarajiwa kufika vyuo vikuu ndani ya miaka michache.
Makamu huyo wa mkuu wa Chuo alisema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na uongozi wa Chuo katika kutoa elimu bora na kuzalisha wataalamu ambao wanatarajiwa kusaidia nchi na jamii katika kuzalisha lakini bado wanakumbana na changamoto za miundombinu kama vile upungufu wa madarasa, maabara na malazi kuweza kukidha idadi kubwa ya wananfunzi wanaojiunga na Chuo.
Aidha Prof. Chibunda alisema chuo kinafanya mikakati ya ndani kuhakikisha kila idara na ndaki zenye uwezo wa kufanya kazi ya uzalishaji mali na bidhaa zenye ubora zinawezeshwa ili kuwapa nafasi wanafunzi kujifunza lakini pia kuongeza mapato ya Chuo kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kimataifa kupitia wataalamu wake kwa wananchi.